WANAVYUO NCHINI WAANDALIWE KATIKA KUJIAJIRI-MAJALIWA WAZIRI MKUU


Kassim Majaliwa amesema ni umuhimu mfumo wa ufundishwaji wa
wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ukaboreshwa ili wanapomaliza waweze
kujiajiri.
“Kumekuwa na tatizo kubwa la wasomi wetu kuwa na
mtazamo kwamba wanapomaliza masomo yao lazima waajiriwe. Upo umuhimu wa
kubadili mtazamo huo kwa kuwapa mbinu zitakazowawezesha kujiajiri.”
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Machi 16, 2018) alipokutana
na kufanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Prof. William Anangisye, ofisini kwake mjini Dodoma.
Amesema
wanafunzi hao wanapomaliza wanatarajiwa wawe na uwezo wa kubuni mbinu
mbalimbali za kujiajiri na kuondokana na mtazao wa kusubiri ajira za
kuajiriwa maofisini.
Waziri Mkuu amesema wasomi hao wanaweza
kuchukua kauli mbiu ya Rais Dkt. John Magufuli ya uchumi wa viwanda kwa
kuanzisha kilimo cha mazao mbalimbali yatakayotoa malighafi za
viwandani.
Pia Waziri Mkuu amesema wasomi hao wanaweza kujikita
katika shughuli za uchimbaji wa madini au usindikaji wa mazao
mbalimbali, hivyo tayari watakuwa wamejiajiri kwa sababu ajira si za
ofisini pekee.
Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyestaafu Profesa Rwekaza
Mukandara kwa kazi nzuri aliyoifanya kipindi cha uongozi wake.
Kwa upande wake, Profesa Anangisye amesema mzigo aliopewa wa kuiongoza
taasisi hiyo si mwepesi, hivyo ameahidi kufanya kazi kwa bidii na
hatokwenda kinyume na matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Kiongozi huyo amesema katika kuhakikisha wanaboresha masomo chuo hapo
wameanzisha skuli ya kilimo na uvuvi, hivyo wanatarajia kuanzisha
mashamba ya mfano kwa ajili ya mazao mbalimbali.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980