Chuo Kikuu Dar chapinga kudahili vilaza



SIKU moja baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kutangaza utata wa
udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu, wadau wakubwa wa elimu, wamejitokeza
kupinga hatua hiyo. Wadau hao ni pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) na Baraza la Vyuo vya Ufundi Tanzania (NACTE).
Taarifa ya UDSM Kwa upande wake, UDSM kimeeleza kwamba hakuna mwanafunzi
hata mmoja aliyedahiliwa chuoni hapo, ambaye hana sifa za kujiunga na
chuo hicho.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Florens Luoga aliliambia gazeti
hili jana kuwa chuo hicho kimeweka utaratibu ambao unaweza mwanafunzi
yeyote anayedahiliwa chuoni hapo, awe na sifa zinazohitajika kwa kuwa
hawafanyi biashara.
“Sisi hapa ni wakali kuhusu jambo hilo, tukibaini kuwepo kwa mwanafunzi
ambaye hana sifa tunamfukuza. Hatusubiri TCU iseme...hata tukibaini kuwa
mtu alifanya udanganyifu na alishamaliza chuo, lakini hakuwa na sifa,
tunamnyang’anya digrii tulivyompa,” alisema Profesa Luoga na kuongeza:
“Hiki ni chuo, hatufanyi biashara, sisi kazi yetu hapa ni kuandaa
wataalamu na ndio maana tunakuwa wakali na makini kuhakikisha wanafunzi
tunaowachukua, wote wanakuwa na sifa stahiki”, alisema Profesa Luoga
alisema uhakiki ambao umefanywa na TCU na kutoa idadi ya wanafunzi 224
wanaosoma chuoni hapo, kuhakikisha wanawasilisha ushahidi wa nyaraka
zao, wanaufanyia kazi, kwani kuna uwezekano tume hiyo haina taarifa
kuhusu programu zinazoendeshwa na chuo hicho.
Alifafanua kuwa kuna baadhi ya programu maalumu, ambazo Serikali ya
Tanzania imeingia na nchi nyingine kwa ajili ya kuendesha programu
maalum.
Alisema kozi hizo zimekuwepo chuoni hapo kwa muda wa miaka 40 sasa na
zinafanywa kutokana na makubalino ya Serikali ya Tanzania na nchi
husika.
Alisema chuo hicho kikongwe Tanzania, kutokana na kuwepo makubaliano
hayo kimekuwa kinapokea baadhi ya wanafunzi ambao wanatoka nje ya nchi
na akasisitiza kuwa yawezekana ndio hao ambao TCU imeshindwa kupata
nyaraka zao.
“Yawezekana kuna taarifa ambazo hazijakaa sawa, tumepokea taarifa ya TCU
sisi kama chuo ni jukumu letu kuitekeleza,” alieleza Profesa Luoga.