Walimu waliopunguza umri kukatwa mafao

WALIMU wanaofanya udanganyifu katika taarifa zao za
kiutumishi, kwa lengo la kujiongezea muda wa kuwepo kwenye utumishi wa umma,
kuanzia sasa, watakapobainika, watakatwa mafao yao, kufidia mishahara yote
waliyolipwa katika kipindi chote, walichojiongezea.
Hayo yalibainishwa na Katibu wa
Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Winifrida Rutahindurwa, mjini
Bagamoyo jana alipokutana na walimu wakuu na wakuu wa shule za umma kutoka
wilaya za Bagamoyo na Chalinze.
Lengo la mkutano wake huo,
ilikuwa ni kutoa elimu juu ya wajibu wao kama mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa
mwalimu kwa mujibu wa sheria ya Tume ya Utumishi wa Walimu namba 25 ya mwaka
2015.
Alisema mwalimu atakapoandikiwa
kibali cha kustaafu, TSC pamoja na mfuko wa mifuko ya hifadhi ya jamii wanajikita
zaidi kuangalia taarifa za mwalimu alizojaza awali, wakati anaanza ajira yake
na sio kutegemea taarifa za stakabadhi ya mishahara peke yake.
Rutahindurwa aliweka bayana kuwa
yapo madhara kwa mwalimu ambaye muda wake wa kustaafu utafika lakini akaendelea
kuwepo kazini kwa kuwa wakati wa kuchukua mafao yake, atakatwa mishahara yote
aliyolipwa kwa kipindi chote alichofanya kazi baada ya muda wake wa halali wa
kustaafu kupita.
“Naomba muwaeleze walimu wote
katika shule zenu kuwa utakapoandikiwa kibali cha kustaafu sisi tunaangalia
zaidi taarifa zako ulizojaza wakati unaajiriwa na kibainika umedanganya
utachukuliwa hatua kwa kuwa umemwibia mwajiri,” alisisitiza.
Alisema TSC ina taarifa zote za
walimu walizojaza wakati wa kuajiriwa, hivyo kwa waalimu wote ambao hawakumbuki
taarifa zao wawasiliane na ofisi za tume ya utumishi wa walimu katika wilaya
zao ili kupata uhakika wa tarehe zao za kustaafu.
Alieleza kuwa kuna wakati walimu
walitakiwa kupeleka taarifa zao za kiutumishi kwa waajiri wao, lakini baadhi yao
walipeleka taarifa tofauti na zile walizojaza kwenye mikataba ya kazi, wakati
wa kuanza ajira.
“Kuna baadhi ya waalimu
wanajifanya hawakumbuki walizaliwa mwaka gani wakati walijaza mikataba wakati
wanaanza ajira na wengi wao wamebadilisha taarifa zao na kujipunguzia umri
jambo ambalo ni kinyume na taratibu na sharia,” alisema.
Katibu huyo aliwaeleza waalimu
kuwa kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa walimu namba 25 ya mwaka 2015, wao
ndio mamlaka ya kwanza ya nidhamu kwa walimu.
Hivyo, wanapaswa kuwashauri na
kuwaelimisha waalimu juu ya kanuni na taratibu za kiutumishi badala ya kukaa na
kusubiri wafanye makosa ili wawachukuliwe hatua.
Walimu walionesha kupokea
maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuondoa usumbufu kwa mwalimu pale
anafuatilia masuala yake ya mafao mara baada ya kustaafu.
Walimu hao wametoa pongezi kwa
katibu wa TSC kwa jitihada kubwa anazofanya katika kuhakikisha mashauri ya
walimu yanafanyiwa kazi na maamuzi yanatolewa kwa muda muafaka.
Mbali na walimu, serikali
imekuwa ikisisitiza juu ya watumishi wengine ambao wako kazini huku wakijua
kwamba walipunguza umri wao ili wasifikie mapema muda wa kustaafu, ikisema
kwamba ni kosa la jinai na kuwa baada ya kufuatilia waliopatikana na vyeti vya
kufoji, pia ina mpango wa kugeukia hata waliopunguza umri kazini.