UWANJA WA KARUME KUTOA AJIRA 400
VIJANA visiwani Zanzibar wanatarajia kufaidika na ajira baada ya kumalizika jengo jipya la kisasa la abiria la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.
.jpg?itok=SisSZre1×tamp=1527675787)
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea jengo hilo, Waziri wa Wizara ya Usafirishaji, Ujenzi na Mawasiliano, Sira Ubwa Mamboya, alisema kuwa baada ya kumaliza jengo hilo ajira zaidi ya 400 zitatolewa. Alisema kuwa ajira hizo wanufaika wa mwanzo ni vijana wazalendo ili kupunguza malalamiko ya ukosefu wa kazi kwa vijana. Alisema kuwa amefurahishwa na hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa jengo hilo ambalo litasaidia kuongeza mapato. “Leo nimefika hapa kuangalia hatua za ujenzi zinavyoendelea kwa kweli nimefurahishwa, kazi nzuri imefanyika na inaendelea kufanyika na matumaini yangu kuwa jengo hili litamalizika katika muda mwafaka uliopangwa,”alisema. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Said Ndumbogani, alisema kuwa jengo hilo litakapomalizika litaweza kupokea abiria wengi zaidi wakiwamo watalii. Alisema kuwa kwa sasa uwanja huo unapokea abiria milioni 1.2 kwa mwaka hivyo matarajio yao ni kwamba wataongezeka. Kwa upande wake, mratibu wa ujenzi wa jengo hilo, Yasser De Costa alisema likikamilika litakuwa na uwezo wa kupokea abiria, milioni 1. 6 kwa mwaka baada ya kukamilika. Alisema kuwa jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuegesha ndege sita zenye uwezo wa kupakia abiria 300 kwa wakati mmoja.