Uncategorized
Maombi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu yamefunguliwa rasmi May 10, 2018 hadi July 15, 2018.
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeongeza idadi ya wanafunzi watakaonufaika na mikopo hiyo kutoka 33, 000 hadi 40,000 kwa mwaka wa masomo 2018/19.
Akizungumza leo, Mei 10, na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdurazaq Badru amesema kwa mwaka wa kwanza wanafunzi 40,000 watapata mikopo ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 7,000 ikilinganishwa na 33,000 waliopata mwaka jana.
“Kwa mwaka huu jumla ya Sh 437 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mikopo hiyo,” amesema
Kadhalika Badru, amesema Bodi hiyo imefungua dirisha la kupokea maombi ya mikopo , zoezi ambalo litafanyika miezi miwili kuanzia leo.
Amesema mwaka huu kipaumbele kitawekwa kwenye kozi ambazo zina uhaba wa wataalam pamoja na zile zenye mchango katika viwanda.
"Katika kuhakikisha dhamira ya serikali ya kuwa Tanzania ya viwanda inatimia, tutaweka kipaumbele kwenye kozi ambazo zitazalisha wataalam,” amesema.
Badru amesema mwaka huu pia bodi imeongeza wigo wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada.
Amesema hapo awali ngazi ya stashahada walikuwa wanapewa mikopo wale wa kozi za ualimu pekee ila sasa maeneo yenye uhitaji wa wataalam nayo yatapewa fursa hiyo.