Bwana
wetu Yesu Kristo mfufuka, alipowatokea wanafunzi wake wakiwa
wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, aliwasalimu na kujifunua kwao
kwa salaamu ya kuwatakia amani.
Wapendwa
watu wa Mungu, katika umoja wetu, sisi maaskofu wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), tunawasalimuni nyote kwa kuwatakia amani.
Bwana wetu Yesu Kristo Amefufuka kweli kweli -Haleluya!.
Yeye ni amani yetu, na pia ni amani kwa watu wote wenye mapenzi mema.
Kwa kufufuka kwake, upendo umeishinda chuki; unyenyekevu umeushinda
ubabe; nuru imelishinda giza; haki imeshinda udhalimu; msamaha umeshinda
visasi; ujasiri umeshinda hofu; na kwa hiyo uzima umeshinda kifo.
Mwaka
2017, Kanisa letu limeadhimisha miaka 500 ya Matengenezo ya Kanisa.
Tukiwa wana Matengenezo tumekumbushwa tena kuwa mwanadamu anaokolewa kwa Neema ya Mungu tu: Wokovu Hauuzwi; Mwanadamu Hauzwi wala kununuliwa; na Uumbajihauuzwi. Kanisa zima na dunia kwa ujumla tunaitwa kusimama pamoja na kuueleza ukweli huu unaoziweka huru dhamiri zetu (Yohana 8:31-32).
Matengenezo
(Reforms) ni dhana ya kibiblia. Tangu zama za Agano la Kale, Mungu kwa
nyakati mbalimbali aliteua wajumbe wake kuwasilisha ujumbe wake kwa
jamii na kwa watawala wa dunia. Kwa Umungu wake, aliwainua wanawake na
wanaume kwa makusudi ya kutoa unabii yaani, ujumbe wa Mungu kwa jamii au
watawala. Wakati mwingine aliinua manabii kuwasemea wasiokuwa na sauti.
Unabii na Matengenezo ni njia ya Mungu katika kusimika utawala wa haki
na unaostawisha uhuru na amani.
Kwa
namna ya pekee, manabii kama Daniel, walionya juu ya uongozi unaojenga
uhalali wake katika wingi wa watu wanaokubaliana na uongozi huo hata
kama ni katika makosa. Haikuwa rahisi kibinadamu kuukosoa mfumo kama huo
lakini Mungu alitumia manabii kuzungumza na mfumo wa namna hiyo. Unabii
wa Daniel 3:7 unasema, “Kwa hiyowatu WOTE, mara waliposikia sauti za baragumu, filimbi, kinubi,zeze, santuri, zumari, na sauti za ala nyingine za muziki,walianguka kifudifudi na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayoMfalme Nebkadneza aliisimamisha”. Hapa
tunaona kosa la kiongozi kutengeneza sanamu, linasababisha kosa la watu
wanaokubali kuiabudu hiyo sanamu. Tumetafakari na kusadiki kuwa, kosa
la kiongozi au mfumo, haliwaondolei hatia wanaomfuata kiongozi au
kuufuata mfumo, hata kama watu hao walikula kiapo cha kutii maongozi ya
kiongozi huyo na mfumo wake. Mbele ya Mungu hakuna ile kanuni ya
kuwajibika kwa pamoja. Kila mtu kwa dhamiri yake anawajibika mbele za
Mungu. Kwa upande mwingine, pamoja na uwajibikaji wa mtu binafsi, Nabii
Ezekieli anatukumbusha na kutuonya kuwa tusipoonya na kusimama katika
zamu yetu, hatia na damu ya wasio na hatia, itadaiwa mikononi mwetu
(Ezekiel 33: 8-9).
Adhimisho
la kufufuka kwa Yesu Kristo (Pasaka) na maadhimisho ya miaka 500 ya
Matengenezo ya Kanisa, yanatusukuma kutafakari utume wa Kanisa katika
jamii kwa nyakati zetu. Tunaalikwa kupeleka ujumbe wa amani kwa watu
wote na kusimama kwa ujasiri katika kuwasemea wasio na sauti katika
jamii ili kuenzi roho ya Pasaka na Matengenezo katika nyakati zetu. Kama
Kanisa na kwa nafsi zetu mmoja mmoja, tunaitwa kwa upande mmoja,
kufundisha, kushauri na kutia moyo. Kwa upande mwingine, tunaitwa
kuonya, kukaripia, kukemea na kuelekeza kwa uvumilivu wote na upendo (2 Timotheo 4: 1-5).
Wajibu
huu kwetu sisi maaskofu ni wito na utume usiokwepeka; na kwa watu wote
wa imani, wajibu huu hauna mbadala. Tunaagizwa kuchochea ujenzi wa
madaraja ya maridhiano katika upendo na amani, na kuwa kinyume na mifumo
yote inayoendeleza chuki na marafakano. Kwa kufanya hivyo, imetupasa
kusema wazi wazi ujumbe wa amani, upendo, heshima, utu, ustahimilivu na
maelewano. Mfumo wowote unaojengwa katika utii wa sheria bila upendo;
heshima bila uhuru; na amani bila haki, unajengwa katika msingi usio
imara. Kupuuza wito huu kuna madhara kwa jamii yetu. Ni sawa na kujenga
nyumba juu ya mchanga (Mathayo 7: 26). Tunasihi kwa machozi mengi, tuwe
wajenzi wenye akili wajengao nyumba zao juu ya mwamba (Mathayo 7:24).
Mwamba tunaotakiwa kujenga taifa letu lenye dini mbalimbali, vyama
mbalimbali, na makabila mbalimbali, umetajwa katika sala kuu ya taifa
letu, yaani, "DUMISHA UHURU NA UMOJA". Bila
Uhuru hakuna umoja uwezao kuleta maendeleo; na bila umoja wa kitaifa,
uhuru wetu hauleti amani endelevu. Kwa sababu ya nguvu ya dhamiri safi
iliyo dira ya taifa letu, tunalazimika kumtii Mungu kuliko mwanadamu
(Matendo 5:29).
B. TAIFA LETU NA AMANI YETU
Tunapoadhimisha
sikukuu ya kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, tunatambua
kuwa utume wa Kanisa letu katika taifa letu, unafanyika katikati ya
changamoto kadhaa. Kwa kuwa Kanisa ni sehemu ya jamii, linaguswa na
changamoto hizo. Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa letu, sisi
maaskofu wa KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia ya
salaam za Pasaka, tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze mzigo wa
kuliombea taifa letu na viongozi wake.
1. Jamii na Uchumi
Kiini
cha Utume wetu katika jamii kinatuingiza kwa nia njema katika maisha ya
uchumi na mshikamano wa kijamii. Neno la Mungu linatufundisha kuwa "Mwanadamu hawezi kuishi kwa mkate peke yake" (Luka 4:4). Pia neno la Mungu linatuhakikishia kuwa Bwana wetu Yesu Kristo alikuja ili tuwe na uzima tele (Yohana
10:10). Tunawiwa katika umoja wetu wa ubaba, kuipongeza serikali yetu
kwa jitihada inazofanya kuboresha maisha ya wananchi. Tumeshuhudia
jitihada na nia njema kuhusu uvunaji na umilikaji wa raslimali za nchi
kwa manufaa ya taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa
kodi ili kuiwezesha serikali kugharamia huduma za jamii. Hata hivyo,
bila kukatisha tamaa jitihada hizo, tunawiwa kushauri yafuatayo:
I.
Sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo, si washindani
wa serikali katika kuchangia maendeleo ya taifa. Mazingira yasiyo
rafiki kuhusu wadau hawa, ni kikwazo kisicholeta mshikamano kati ya
serikali na sekta binafsi na mashirika ya dini katika kuleta maendeleo.
Jitihada za makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya
ushindani kati ya serikali na wadau hawa ili kuimarisha mahusiano mema
kati ya serikali na sekta binafsi.
II.
Ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe endelevu; jitihada za kukusanya
kodi ziendane na elimu kwa mlipa kodi. Msisitizo wa uzalendo wa kulipa
kodi uende sambamba na ustawi wa walipa kodi katika shughuli zao za
biashara. Mivutano isiyo na tija kati ya walipa kodi (wafanya biashara)
na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui unaopunguza
makusanyo ya kodi na kujenga ushawishi wa rushwa. Mfumo wa kodi
unaowafilisi wafanya biashara, haulengi kujenga uchumi wa viwanda.
III.
Kutokana na ongezeko kubwa la vijana wasio na ajira; jitihada za wazi
na za makusudi zifanyike ili msukumo wa uchumi wa viwanda ufikie
matumaini yanayoshikika miongoni mwa vijana wasio na ajira. Sekta
binafsi, wawekezaji na wadau wengine, wahakikishiwe usalama wa mitaji
yao kisheria. Hili likifanyika ni kichocheo kizuri cha ujenzi wa
viwanda.
IV.
Uchumi wa viwanda (vidogo na vikubwa) uendane na uwekezaji katika sekta
ya kilimo maeneo ya vijijini. Kilimo na ufugaji ndizo sekta zenye wigo
mpana wa viwanda vinavyogusa maisha ya watanzania walio wengi. Utozaji
holela wa kodi na ushuru wa mazao unakatisha tamaa wadau wa kilimo.
Migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja, na
wakulima/wafugaji na wawekezaji kwa upande wa pili, si kivutio cha
uwekezaji katika sekta ya kilimo.
2. Maisha ya Siasa
Kwa
umoja wetu katika utume, tunatambua siasa safi na uongozi bora kuwa ni
misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa letu. Ujio wa vyama
vingi mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii bali ulipanua
matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo. Taifa ni
mkusanyiko wa taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa
njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu ya
vyama, taasisi na makundi.
Taifa
huongozwa na katiba iliyo kiini cha sheria zote. Taifa haliongozwi na
ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani za vyama. Serikali
huongozwa na katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi na tunu za
taifa). Serikali husimamiwa na bunge huru lililo sauti ya wananchi.
Wananchi ndilo chimbuko la madaraka ya bunge. Bunge halisimamiwi na
ilani, chama chochote wala mtu awaye yote. Kwa umoja wetu na kwa nyakati
zetu, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi
iliyolilea taifa letu. Baadhi ya matukio hayo ni:
I.
Hofu iliyojengwa katika matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji,
kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa,
mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na
matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.
II.
Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru wa kujieleza, kukusanyika, na
kupata habari. Kwa mwenendo huu, kuna hofu kuwa hata uhuru wa kuabudu
uko mashakani.
III.
Kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na
Tume ya Uchaguzi. Hatua hii ni pamoja na kudhoofishwa kwa serikali za
Mitaa.
IV.
Kukosekana kwa mazingira ya haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa
katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote zimeghubikwa na ubabe, vurugu,
hila, na vitisho.
V.
Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi. Hatua
hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa letu na kukuza
migawanyiko.
VI.
Kushamiri kwa chuki mioyoni mwa watu ambalo ni chimbuko la visasi,
kukata tamaa, na ushiriki mdogo wa wananchi katika chaguzi na maisha ya
siasa.
VII. Udhalilishaji wa kauli njema isemayo "Maendeleo hayana chama".
Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia fedha nyingi katika
chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili kuleta
maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu
anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama
kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa,
kujeruhiwa na uharibifu wa mali.
Mambo haya ni tishio linalohatarisha umoja na amani ya nchi yetu.
3. Masuala Mtambuka
Kanisa
ni alama ya uwepo wa utume wa kuleta na kutunza matumaini katika jamii.
Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa jamii ni ukwepaji wa wajibu
wake. Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na mtu isipokuwa Mungu
tu, ni chachu ya amani na matumaini. Kwa dhamiri safi inayotokana na
utambuzi wa "Wakati wa Mungu"(Kairos)
katika taifa letu, tunawiwa kutambua masuala mtambuka yanayogusa maisha
ya watu kipekee na kwa njia nyingi na kuyatolea ushauri ufuatao:
I.
Kuhitimisha mabadiliko ya mara kwa mara katika mfumo wa elimu nchini
ili kuondoa mwanya wa kila mtendaji mkuu wa wizara kuja na sera yake.
Elimu ni kitovu cha ustawi wa taifa, kisiwe kinachokonolewa chokonolewa
kila wakati. Sekta zote nchini hujenga mafanikio yake katika mafanikio
ya mfumo thabiti wa elimu.
II.
Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya elimu ya juu uwe shirikishi na
usiokuwa na "ubaguzi" kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa
serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma
shule binafsi na wale wa shule za serikali, n.k. Kwa kuwa huu ni mkopo,
jitihada ziwekwe zaidi katika urejeshaji wa mkopo huo kwa kuzingatia
kuwa huu ni mkopo kwa mtoto siyo kwa mzazi.
III.
Vyombo vya usimamizi wa sheria na utoaji haki vionekane vinatenda haki
sawa kwa watu wote na makundi yote bila kuacha ishara za fadhila au
kukomoana.
IV.
Wajibu wa serikali kikatiba katika kulinda uhai wa raia wake, uonekane
unatekelezwa bila kuacha mwanya wa kuituhumu serikali. Ukiachwa mwanya
katika ulinzi wa uhai wa raia, waweza kutumiwa na mamluki kujichukulia
sheria mkononi kwa niaba ya serikali. Damu isiyo na hatia
ina
madhara kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo. Mpaka sasa tumeshuhudia
umwagaji wa damu unaotusuta sisi sote na mamlaka zote. Mungu anatusuta
watanzania kama alivyomsuta Kaini: "Sauti yadamu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi" (Mwanzo 4:10).
V.
Uhai wa mtu una thamani isiyopimika. Ni wajibu usiokwepeka kuulinda na
kuutunza uhai kwa vitendo halisi. Endapo uhai umepotea katika mazingira
yoyote, uchunguzi huru na wa haki ufanyike na taarifa zitolewe kwa
wakati muafaka ili kujenga jamii yenye imani kwa serikali na vyombo
vyake. Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya raia, majaribio ya
kuwaua wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na kutolewa
taarifa, ni shina la hofu na uchungu katika jamii. Jamii iliyojaa hofu
na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo wala kuwa na roho ya uzalendo.
VI.
Ili kulipatia taifa letu ufumbuzi wa mambo yote tuliyotaja na kushauri
kwa wakati huu na ujao; tunaisihi serikali ya awamu ya tano, kurejea
mchakato wa upatikanaji wa KATIBA MPYA ya wananchi, iliyopendekezwa na
wananchi kupitia Tume ya Warioba. Watanzania wengi wanaona na kuamini
kuwa KATIBA MPYA ina majibu ya kukidhi mahitaji ya taifa letu kwa sasa
na baadaye. KATIBA MPYA ni zao la utashi wa Watanzania kupitia tume ya
Warioba iliyokuwa na uwakilishi mpana wa taifa letu.
VII.
Aidha, tunawashauri raia wema, kwa njia za kidemokrasia kupitia
majukwaa ya kikatiba yaliyo katika maeneo yao, kudai upatikanaji wa
KATIBA MPYA. Itapendeza ikiwa KATIBA MPYA itapatikana kabla ya uchaguzi
mkuu ujao. Mambo mazuri yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano
yatadumu iwapo kuna KATIBA MPYA inayolinda mazuri. Kiongozi mzalendo si
mbadala wa KATIBA MPYA. Tanzania yenye amani na maendeleo ni tunda la
itikadi zote, dini zote, makabila yote na makundi yote chini ya KATIBA
MPYA.
C. HITIMISHO
Kufufuka
kwa Yesu Kristo ni kiini cha Matengenezo ya Kanisa. Kwamba, katikati ya
jamii iliyokata tamaa na kutawaliwa na hofu, Kristo alifufuka na kuleta
matumaini mapya. Kwamba, katikati ya wasiwasi wa Kanisa kupoteza nguvu
ya utume wake, Roho Mtakatifu aliongoza Matengenezo ya Kanisa. Kwa hiyo
Matengenezo ni endelevu katika jamii ya watu na taasisi zao. Muasisi wa
Matengenezo Dr. Martin Luther yungali analiwajibisha Kanisa kuzingatia
utume wake unaoleta matumaini mapya kila siku. Waliobatizwa wote ni
wamisionari tunaotumwa na Bwana wetu Yesu Kristo (Yohana 20:21).
Imetupasa kuwa nuru na chumvi ya jamii na kuwa mawakala wa uhuru, umoja
na amani.
Taifa
letu lilipata uhuru mwaka 1961 bila kumwaga damu. Roho ile ile ya
majadiliano na maridhiano iliyokuwamo ndani ya waasisi wa taifa letu,
inatakiwa kila wakati. Uhuru ulioletwa kwa majadiliano, utunzwe na
kulindwa bila ulazima wa kumwaga damu ya watanzania. Uhuru naUmoja ndizo ngao zetu zilizolitunza taifa kwa zaidi ya miaka 50.
Sisi
tulio maaskofu kwa neema ya Mungu, tunaleta wito kwenu wenye imani
katika dini mbalimbali, kuliombea taifa letu. Kuwaombea wote wenye
madaraka ili wajaliwe hekima, busara na upendo kwa taifa na watu wake.
Kupitia jumuia ndogo ndogo na sharika zote, waombee viongozi wetu ili
Mungu awajalie na kuwatunuku kiu ya kutenda haki, kusikiliza kuliko
kusema, kuelekeza kuliko kuamrisha, kuunganisha kuliko kutawanya,
kupenda watu kuliko kutamani kupendwa na watu, kutamani kutumika kuliko
kutumikiwa (Marko 10:45), kuheshimu kuliko kuheshimiwa.
Ujumbe
wa Pasaka unatuhimiza kuthamini uhai. Bwana wetu Yesu Kristo alikubali
kufa ili kuhifadhi uhai wetu. Kwa kufa kwake na kufufuka, amekomesha
kifo na mawakala wake. Tunaitwa kuthamini uhai na kutoruhusu tena watu
kuteswa na kuuawa. Kwa hekima yote na unyenyekevu, tunasihi tena, kwamba
ikubalike kuwa hitaji la watanzania walio wengi kwa sasa ni KATIBA
MPYA. Katiba Mpya ipatikane ili kukuza na kuimarisha mfumo wa utawala
utakaolinda uhai wa watu, raslimali za nchi, tunu za taifa, uhuru wa
mihimili ya dola, na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.