Diamond, Vanessa Mdee, Aslay na Wengine Kibao Wamlilia mwanafunzi NIT
Kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kilichotokana na kupigwa risasi na polisi juzi kimewaibua wasanii maarufu nchini ambao wamelaani tukio hilo.
Akwilina Akwiline alipigwa risasi akiwa kwenye daladala wakati polisi walipowatawanya wafuasi wa Chadema.
Wasanii Vanessa Mdee, Diamond Platnumz, Jackline Wolper, Steve RnB, Martin Kadinda, Wakazi, Aslay, Juma Nature na mwanamitindo Tausi Likokola.
Diamon na Aslay Isihaka wameandika ujumbe wakitoa pole kwa familia na kumuombea Akwilina apumzike kwa amani.
Vanessa Mdee kupitia mtandao wa Instagram alisema, “Huwa sizungumzii siasa wala sijihusishi na masuala ya kampeni za siasa na sijawahi kufanya na sitoanza leo. Ila siku zote nazungumzia masuala ya vijana hasa watoto wa kike maana I’m passionate about the girl child. Leo naiombea familia ya Akwilina, ndugu, jamaa na marafiki zake wote. Mungu awafanyie wepesi. pumzika kwa amani.”
Mwanamitindo Tausi Likokola ambaye makazi yake yapo nchini Marekani katika waraka wake amesema amesikitishwa na tukio hilo kwa kuwa ni pigo katika jitihada za kumkomboa mtoto wa kike na ndoto za binti huyo zimezimwa ghafla.
“Nimeamka na kukutana na habari za kusikitisha, ukweli Akwilina anahitaji kupata haki yake kwa kumtambua aliyefanya hivyo na afikishwe katika mikono ya sheria,” alisema.
Amesema matukio kama hayo yanapaswa kupingwa kwa nguvu zote kwa kuwa yanachafua jina la Tanzania ambayo zamani ilipigiwa mfano kama Kisiwa cha Amani.
Mwigizaji Jackline Wolper aliandika, “Nimejikaza nikae kimya, lakini naona kama nataka tu kuongea kuhusu suala la mwanafunzi aliyeuawa bila hatia! Mtoto wa watu ambaye alikuwa na ndoto zake nchini kwake ameiacha Tanzania yake! Wewe uliyefanya kitendo hiki kwa binti wa watu sikuombei ufe wala uhukumiwe.”
“Unaua mtu kisa umepewa madaraka ya kutumia bunduki? Unaua watu kwa ajili ya mambo ya kisiasa? Huu ni uonevu na ukosefu wa maarifa. Aiseee nimeumia kwa sababu nilisikia jana bunduki zikipigwa nikiwa ofisini kwangu kila mtu anakimbia yaani ilinijia picha ya Iraq na si Tanzania ile nilioizoea, kila mtu anafunga biashara zake na wengine wanaacha biashara zao wanakimbia daaah imeniuma sana,” aliandika na kumalizia na hashtag akisema siasa zisituharibie nchi.
Mwanamuziki Steve RnB aliandika: “Nahisi ifike kipindi tuangalie ni mangapi yanaigharimu nchi kwa sababu tu ya siasa hizi. Siasa kama haziwezi kuendeshwa bila ya kumwaga damu hadi kwa watu wasiokuwa na hatia inaonyesha ni jinsi gani hatujakua kisiasa. Aliyefanya hivyo Mungu atamhukumu.”
Mbunifu wa mitindo, Martin Kadinda aliandika akisema, “Kwa ninavyoamini kila tunapopoteza yule tumpendaye duniani basi tunaongeza malaika anayetujua, Aquillina amerudi ambapo wote tutarudi. “
Shilole aliandika, “Tumbo la uzazi limeniuma jamani. Pumzika kwa amani katoto kazuri kasikokuwa na hatia.”
Rapa Wakazi akizungumzia tukio hilo katika akaunti ya Instagram aliandika, “Pumzika kwa amani. Nchi za watu damu inamwagika ili haki ipatikane ukiondoa matukio ya uhalifu. Sasa kwetu damu inamwagwa na wale wenye wajibu wa kulinda haki na amani yetu.
Chanzo: Mwananchi