-->

FANIKIWA SASA JINSI YA KUGAWA MATUMIZI YÀ FAIDA KATIKA BIASHARA


Watu wengi wanapoingia kwenye biashara, hufikiri ya kwamba biashara ndiyo mwisho wa kila kitu. Kwa kuwa sasa wao ndiyo wamiliki wa biashara, basi wana uhakika wa kipato maisha yao yote. Lakini hii siyo kweli mara zote, hata biashara ambayo tayari inajiendesha vizuri, inaweza kukutana na changamoto na kusuasua au hata kufa kabisa. Yapo mambo mengi yanayoweza kutokea kwenye biashara ambayo yanaweza kuzima ndoto zako za kuwa na kipato cha uhakika.
Wafanyabiashara wengi pia wamekuwa hawafuatilii kwa karibu faida wanayopata kwenye biashara zao. Wao wanachofanya ni kuuza na kununua, au kuzalisha na kuuza. Kadiri wanavyoona fedha zipo na bidhaa zipo, basi hicho ni kiashiria kizuri cha biashara kwenda vizuri. Ni wafanyabiashara wa aina hii ambao jambo lolote likitokea kwenye biashara, wanabaki wakiwa watupu kabisa, ni kama wanaanzia chini kabisa.
Ili kuepuka changamoto hizo za kibiashara, leo tutakwenda kujifunza namna ya kupangilia matumizi ya faida unayoipata kwenye biashara yako.
Kabla ya kujua utumieje faida yako, kwanza lazima ujue ni faida kiasi gani unapata. Lazima usimamie biashara yako vizuri, uifuatilie kwa karibu na upige hesabu zako vizuri sana na kwa umakini. Lazima ujue kila kinachoingia na kila kinachotoka kwenye biashara. Na hii yote lazima iwe kwa maandishi au mfumo wowote unaoweka kumbukumbu za biashara vizuri. Kwa njia hii unaweza kuona faida unayopata ni kiasi gani na inatoka wapi.
Baada ya kujua faida, hapo sasa unaweza kuigawa vizuri ili kuhakikisha biashara inaendelea na mambo yako mengine yanaendelea.
Sehemu ya kwanza ya matumizi ya faida ya biashara ni kuwekeza kwenye biashara hiyo na kuikuza zaidi. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiangalia kipi kimepungua au kuisha na kukiongeza, lakini wamekuwa hawaangalii kipi kipya cha kuanzisha, au namna gani ya kukuza biashara zaidi. Hii inawapelekea kubaki pale walipo na kuwa kwenye hatari ya kupoteza biashara zao hasa pale ushindani unapoibuka.
Unahitaji kuwa unaangalia maeneo mapya zaidi ya kukuza biashara yako, labda bidhaa au huduma mpya ambazo hujaanza kutoa sasa lakini zina uhitaji. Au labda lipo eneo jipya ambalo unaweza kuanzisha biashara yako pia. Kwa vyovyote vile angalia namna unavyoweza kuikuza biashara yako zaidi.
Ni muhimu kuhakikisha unakuwa na kiwango fulani cha faida ambacho unakiwekeza kwenye biashara yako. Inaweza kuwa asilimia 30 ya faida unayopata, inakwenda kwenye kukuza biashara yako zaidi. Hiki ni kipaumbele kikubwa kwa sababu ndiyo itakutoa hapo ulipo sasa na kufika mbali zaidi.
Sehemu ya pili ya kupeleka faida yako ni uwekezaji nje ya biashara. Unahitaji kuwa na uwekezaji nje ya biashara unayofanya sasa. Uwekezaji ambao utakutengenezea kipato bila hata ya kufanya kazi moja kwa moja. Kama ulikuwa hujajua bado, ili kufikia utajiri, ili kuwa na uhuru wa kifedha, unahitaji kuwa na vyanzo vingi vya kipato. Biashara yako hata kama ina faida kiasi gani, pekee haitoshi kukupa uhuru wa kifedha, lazima uwe na vyanzo tofauti. Hii inakulinda pale chanzo kimoja kinapokuwa na changamoto, vyanzo vingine vinaendelea kuzalisha.
Sehemu ya tatu ya kupeleka faida yako ni matumizi yako binafsi. Huenda unategemea biashara yako katika kupata fedha za kuendesha maisha yako. Sasa hapa unahitaji kutumia sehemu ya faida yako kupata mahitaji yako. Usitumie faida yote, kwa sababu kuna hayo mengine muhimu ya kufanya. Tumia sehemu ya faida, labda asilimia 30 au 40 ya faida. Na kama hiyo haikutoshi, basi kazana upate faida zaidi ili uweze kupata zaidi ya matumizi.
Matumizi sahihi ya faida unayopata kwenye biashara yako ndiyo yatakayokuwezesha kutoka kwenye biashara uliyopo sasa mpaka kuwa na biashara nyingi na kubwa zaidi. Simamia vizuri matumizi ya faida yako ili kuweza kufikia ndoto zako.
Kupata ushauri bora kabisa wa kuanza na kukuza biashara yako, bonyeza maandishi haya kupata maelekezo. Karibu ushauriwe vizuri ili uweze kukuza biashara yako na kuondokana na changamoto.
PENDA BIASHARA, JIFUNZE BIASHARA.


Read also-: