CWT yaunga mkono juhudi zinazofanywa na Makamu wa rais Samia Suluhu.
Katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na makamu wa rais wa jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha suala la
kufanya mazoezi kwa lengo la kuboresha afya za watanzania chama cha
walimu Tanzania (CWT) kimekabidhi vifaa vya michezo kwa shule 15 za
msingi na sekondari zilizo katika halmashauri ya wilaya ya bukoba
iliyoko mkoani Kagera.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni mipira ambayo itatumiwa na walimu pamoja na
wanafunzi kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mchezo wa mpira wa miguu,
mpira wa pete, mpira wa wavu na mpira wa mikono, vifaa hivyo
vimekabidhiwa leo na mwenyekiti wa chama cha walimu wa wilaya ya
Bukoba, Methodius Majojo wakati wa hafla fupi iliyofanyika kwenye
viwanja vya ofisi ya chama hicho ambaye ameahidi kuwa zoezi la kugawa
vifaa vya michezo kwamba litakuwa endelevu.
Kwa upande wao baadhi ya walimu wa shule 15 zilizopata vifaa hivyo kwa
nyakati tofauti wamepongeza uamzi wa CWT wa kuunga juhudi za makamu wa
Rais za kuhamasisha suala la mazoezi hivyo wakaziomba taasisi nyingine
ziige mfano wa chama hicho huku wakionyesha imani yao kuwa kupitia
michezo wanafunzi watajengeka kitaaluma zaidi.