Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo hatarini kupata maambukizi ya ebola, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) umeanza kutumia vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuwabaini wenye ugonjwa.
Vifaa hivyo ambavyo kitaalamu vinaitwa thermal scanner, vimeanza kutoa huduma na jana naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alifika kujionea.
Juzi, WHO ilisema Tanzania ni nchi iliyopo kundi la pili la zilizo katika hatari ya kupata maambukizi ya ebola kwa kuwa inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC). Mpaka sasa watu 27 wameripotiwa kufariki dunia nchini humo kwa ugonjwa wa ebola.
Akizungumza jana, ofisa afya mfawidhi wa JKIA, George Ndaki alisema wamekuwa na maandalizi ya msingi ambayo wanahakikisha abiria wote ndani ya uwanja huo wanakuwa salama.
Alisema Serikali imewapa vifaa vya kisasa vinavyoweza kubaini mtu yeyote mwenye virusi vya ebola kupitia joto lake la mwili.
“Iwapo tutambaini mgonjwa yeyote kuna vyumba vimetengwa tutamwingiza hapo na tukijiridhisha tutambeba kwa magari yetu ya wagonjwa yaliyopo hapa,” alisema Ndani.
Alisema wametenga eneo maalumu kwa ajili ya wagonjwa wa ebola ingawa mpaka sasa hakuna mtu aliyebainika kuwa na ugonjwa huo hapa nchini.
Akizungumzia udhibiti huo akiwa JNIA, naibu waziri wa Afya, Dk Ndugulile alisema ameridhishwa na ukaguzi unaofanywa na kwamba mipaka ya nchi nzima iko salama. Dk Ndugulile alifanya ziara kukagua namna ambavyo uchunguzi unafanyika kwa abiria wote wanaoingia nchini kupitia mashine maalumu zinazochunguza joto la mwili.
Pia, alisema amejiridhisha na maandalizi ambayo yanaendelea na endapo akitokea mgonjwa wa ebola Tanzania imejidhatiti kupambana na ugonjwa huo.
“Tumefunga mashine za kisasa kabisa za kuangalia kwa kila abiria anayeingia hali zao za joto na wale wote tunaowabaini kwamba joto lao limeongezeka tumeweka mfumo wa kufanya uchunguzi zaidi kwa kuwatengea maeneo yao mahsusi,” alisema.
Dk Ndugulile alisema kwa wale ambao watabainika kwamba wana joto la juu na watakuwa wametoka katika nchi ya DRC watawachukua na kuwekwa katika sehemu maalumu kuwafuatilia ili kujua hali zao kiafya.
Alisema mbali na viwanja vya ndege, wizara hiyo imehakikisha maeneo yote ya mipaka yanalindwa.
“Tumesambaza vifaa vyote vya kujikinga katika maeneo yetu ya mipaka. Pamoja na hilo tumefanya mazoezi ya kujikinga, tunaendelea kutoa elimu kwa jamii nzima ya Watanzania na kuendelea kulinda mipaka yetu yote,” alisema.
Ndani ya uwanja huo wa ndege eneo wanaoloingilia abiria, Mwananchi lilishuhudia mashine zikiwa zimewekwa katika milango yote inayotumika kuingilia huku abiria wakipita na kukaguliwa na mashine hizo bila wenyewe kujua.