HESLB kupokea maombi ya mikopo Mei
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) mwezi ujao itaanza
kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/19.
Upokeaji maombi utaanza Mei, 2018 baada ya kukamilisha uboreshaji wa mfumo wa uombaji kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru katika taarifa aliyoitoa
leo Jumanne, Aprili 17, 2018, amesema maombi yote yatapokewa kwa njia
ya mtandao (www.olas.heslb.go.tz) ambao umeboreshwa na Kituo cha
Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM).
Badru amesema pia watatangaza mwongozo wa kina utakaotoa utaratibu wa
kuwasilisha maombi; tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi; sifa na
vigezo vitakavyotumika katika kuchambua na kutoa mikopo kwa mwaka ujao
wa masomo unaotarajiwa kuanza Oktoba, 2018.
“Tunawasihi wote wanaotarajia kuomba mkopo wa elimu ya juu kusoma kwa
makini mwongozo tutakaoutoa kwa vyombo vya habari na tovuti mwanzoni mwa
Mei, 2018 na kuuzingatia,” amesema Badru.
Amesema mwaka jana zaidi ya waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi ya
61,000 hawakuambatisha nyaraka muhimu kama vile vyeti vya kuzaliwa au
hata vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (Rita) kama ilivyoelekezwa.
Nyaraka nyingine ambazo waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni nakala za
vyeti vya kitaaluma za kidato cha nne; cha sita na stashahada ambazo
zimethibitishwa na kamishna wa viapo yaani wakili au hakimu.
Badru amesema wanafunzi waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye
ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa
mganga mkuu wa mkoa, wilaya au kituo cha afya cha Serikali.
Amesema wanafunzi waliofadhiliwa katika masomo ya sekondari au
stashahada (diploma) wawe na barua za uthibitisho wa udhamini huo kutoka
taasisi zilizogharamia masomo yao.
Badru amesema maofisa wa HESLB watatembelea mikoani kukutana na waombaji
wa mikopo kuwaelimisha kuhusu utaratibu sahihi wa kuwasilisha maombi ya
mikopo kwa njia ya mtandao.