Profesa Hubert Kairuki kuenziwa kwa shughuli za kijamii
Shirika la Afya na Elimu la Kairuki (KHEN) katika kumuenzi muasisi wa
taasisi hiyo, marehemu, Profesa Hubert Kairuki itafanya mambo mbalimbali
ya kijamii ikiwamo kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa kituo cha
kusaidia watu wenye matatizo ya kupata watoto.
Akizungumza leo Jumapili Februari 4 kwenye mkutano na waandishi wa
habari, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki
Profesa Charles Mgone amesema taasisi hiyo ya Kairuki itaweka jiwe hilo
kwaajili ya kuanza ujenzi wa kituo kitakachotoa huduma kwa wanawake
ambao hawana uwezo wa kushika mimba na wanaume ambao hawawezi kutungisha
mimba kwa njia ya kawaida.
"Kwa sasa kuna changamoto kubwa ya wanawake kushika ujauzito kwa njia ya
kawaida na hata wanaume, katika kumuenzi muasisi wetu tutaweka jiwe
hilo kesho eneo la Bunju" amesema.
Amesema kituo hicho kikikamilika kitakuwa msaada kwa familia ambazo
hazijabahatika kupata watoto kwa njia za kawaida kwani kitahusika na
upandikizaji wa mbegu na ushauri kwa wenye matatizo hayo.
"Mchoro kwaajili ya ujenzi wa kituo upo katika hatua za mwisho na
tayari taasisi hiyo imeandaa wataalamu ambao watatoa huduma hizo pindi
kitakapokamilika" amesema.
Profesa Mgone amesema mbali na hilo pia wataanzisha kliniki ya mama,
baba na mtoto, watatoa huduma za afya bure kwa wananchi wote kuanzia
kesho hadi sita Februari mwaka huu.
‘’Tutakuwa na shughuli nyingi kwa kipindi cha siku tatu kuanzia keshom
tutakuwa na uchangiaji wa damu, tutakuwa na mashindano ya kitaalamu
baina ya wanafunzi wa shule ya uuguzi Kairuki na chuo kikuu cha Kairuki
hayo yote yatafanyika Bunju"amesema.
Amesema watakuwa na upimaji wa shinikizo la damu, uwiano wa urefu na unene na kutoa ushauri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Kairuki, Dk. Asser Mchomvu
akimwelezea marehemu Kairuki aliyefariki Februeri 6,1999 ,amesema
alikuwa na uzalendo na nchi yake alipenda watanzania wapate huduma bora
za afya ndiyo maana aliamua kuanzisha huduma za afya binafsi lengo ni
kusaidia msongamano hospitali za umma.