Mahitaji ya vyuo, kiwanda cha nyama Simiyu
UJENZI wa vyuo mkoani Simiyu ni moja ya fursa kuu kati ya 14 za
uwekezaji zinazopatikana Simiyu kutokana na utafiti wa kisayansi
uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii
(ESRF).
Watafiti hao wanasema kwa sasa kinachohitajika kwa haraka ni chuo cha
kilimo na ufugaji ambacho wanashauri kijengwe katika wilaya ya Busega na
chuo cha teknolojia ya viwanda, wakishauri kijengwe Bariadi palipo
makao makuu ya mkoa.
Kwa mujibu wa ESRF, kutokana na mkakati wa kufanya mabadiliko makubwa
katika kilimo na viwanda, Simiyu inahitaji vyuo hivyo vya kilimo na
viwanda vitakavyozalisha nguvu kazi itakayohitajika sana katika
kuubadilisha mkoa katika maeneo hayo.
Kwamba kutokana na ongezeko la haraka la watu la asilimia 2.8 na hatua
ya serikali kutoa elimu bure, Simiyu haiwezi kukwepa kuhitaji vyuo vya
ufundi vya kutosha na hivyo ni wakati mwafaka sasa kwa watu kuchangamkia
fursa hizo.
Kiwanda cha nyama Fursa nyingine kwa mujibu wa ESRF ambayo wawekezaji
wanapaswa kuimulika ni ujenzi wa kiwanda cha nyama mkoani Simiyu, hatua
itakayotoa soko la uhakika la wafugaji wa ng’ombe na hivyo pia kuwafanya
wafuge kabiashara zaidi.
Simiyu kwa sasa inakadiriwa kuwa na zaidi ya ng’ombe milioni 1.5, wengi
wakiwa aina ya Zebu ambapo asilimia 90 wanafugwa na wananchi lakini bado
wanatoa mazao kidogo.
Kiwanda hiki cha nyama kinashauriwa kwenda sambamba na uwepo wa kiwanda
au viwanda vya kuzalisha vyakula vinavyosaidia kunenepesha ng’ombe
sambamba na kuwepo kwa machinjio ya kisasa. ESRF wanasema ongezeko la
ukuaji wa miji katika mkoa wa Simiyu bila shaka litakwenda sambamba na
ongezeko la mahitaji ya nyama.
Halikadhalika, watafiti hao wanasema kuna soko la kutosha la nyama
katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na hata nje ya Jumuiya hiyo.
Ujenzi wa nyumba nafuu Kwa mujibu wa ESRF, Simiyu pia inahitaju nyumba
za kisasa lakini zenye bei nafuu ambazo wananchi wengi wanaweza
kuzinunua kwa mtindo ambao wajenzi wataona unawezekana.
Watafiti hao wanasema kwa sasa asilimia 40 ya wakazi wote wa Simiyu ni
vijana walio chini ya umri wa miaka 30 ambao katika mwongo mmoja ujao
wataanzisha familia na kuhitaji nyumba za kuishi.
“Simiyu ni mkoa mpya, hivyo kutakuwa na ongezeko la watu wanaohamia
katika mkoa huu kwa ajili ya kufanya kazi, kufanya biashara au kutafuta
fursa hizi na zile. Hawa wote watahitaji nyumba,” inasomeka ripoti ya
awali ESRF ikiwa na kichwa cha habari, ‘Muongozo wa Uwekezaji Mkoani
Simiyu.’
Taasisi za kiserikali kama Shirika la Kiuchumi la Jeshi la Kujenga Taifa
(Suma JKT) na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wanahimizwa na watafiti
kuchangamkia fursa hizo adhimu bila kusahau makampuni binafsi ya ujenzi.
Mbali na hizo fursa zilizojadiliwa hapo juu, fursa zingine ambazo
tumeshaziangalia kwa kina ni uzalishaji wa pamba yenye kiwango bora na
uchimbaji wa mabwawa sambamba na kuendesha skimu za umwagiliaji.
Katika mfululizo huu tuliangalia pia ushauri wa kutenga maeneo au miji,
mawili maalumu kwa ajili ya viwanda, maduka na huduma nyingine za
kifedha na ujenzi wa viwanda vya kisasa vya kuchambua pamba na vya nguo.
Tutaendelea kujadili fursa zingine zilizobaki kwa kina katika jarida la
Uchumi Jumanne wiki ijayo, ambazo ni fursa za huduma za ugani kwa
wanyama (veterinary services), kiwanda cha ngozi na viwanda vya
kuzalisha bidhaa za ngozi, Fursa nyingine zinazopatikana Simiyu
tutakazoziangalia kwa kina ni viwanda vya kusindika mafuta ya kula
yatokanayo na mbegu, viwanda vya maziwa na mazao yake, uwindaji wa
kitalii, bandari, usafiri na michezo ya majini katika wilaya ya Busega.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, ameshaweka wazi kwamba yeyote
mwenye kutaka kuwekeza mradi utakaokuwa na manufaa kwa wana-Simiyu
ikiwemo kutoa ajira kwa vijana, atapewa ardhi bure.
Na tayari Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), inayochapisha magazeti
ya Daily News, Habari- Leo na SpotiLeo, iliandaa Jukwaa la Biashara
lililoketi Februari 13 na kushirikisha wadau muhimu wa maendeleo.
Wakati TSN ikifanya kazi ya kupaza sauti ili wananchi wajue “Simiyu
kunani”, wadau wa jukwaa, hususani taasisi za fedha, TIB na NMB
zilionesha namna watu wanavyoweza kuzitumia kuwekeza Simiyu huku Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) ikieleza namna ya kuhakikisha kodi zinalipwa.