SAUT MWANZA: Serikali Ndiyo Inayopaswa Kuwajibika, Wanafunzi wasio na Sifa za Kujiunga na Vyuo Vikuu



Uongozi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), umesema baadhi ya
wanafunzi walioorodheshwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuwa
taarifa zao za uhakiki zina kasoro hivyo kuwa hatarini kukosa sifa za
kuendelea na masomo, walishamaliza masomo zaidi ya miaka mitatu
iliyopita.
Mbali na kauli hiyo, chuo hicho, vyuo vingine vya elimu ya juu na wadau
wa elimu wameijia juu TCU wakisema taasisi hiyo ndiyo inayopaswa kubeba
lawama.
Juzi, TCU ilitoa orodha ya vyuo 52 ambavyo ilidai wanafunzi wake
walidahiliwa katika masomo ambayo hawakustahili na kutoa muda hadi
Februari 28 kufanya uhakiki vinginevyo watapoteza sifa za uanafunzi.
Lakini jana, uongozi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine ulisema Serikali ndiyo inayopaswa kuwajibika.
Makamu Mkuu wa Saut ambacho kimetajwa kuwa na wanafunzi 1,046 wasiokidhi
vigezo, Dk Thadeus Mkamwa alisema kuwa chuo hicho kilifuata taratibu
zote lakini wameshangaa TCU ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kudahili
wanafunzi, kutoa taarifa zenye mkanganyiko.
mwananchi