Mwenye simu anavyoweza kuhama mtandao na namba


MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imezindua mpango maalum
unaomuwezesha mteja kuhama mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine bila
kubadili namba ya simu, na kueleza hatua 13 za kufuata ili kupata huduma
hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, akizungumza na wahariri
na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jana jijini Dar es Salaam,
alisema huduma hiyo ni ya hiari na ili mtu aweze kuhama mtandao mmoja
kwenda mwingine ni lazima afuate hatua 13.
Mhandisi wa Mawasiliano wa TCRA, Mwesigwa Felician, alitaja hatua ya
kwanza ya kuhama mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine kuwa ni kufika
kituo cha mauzo au kwa wakala anayetambuliwa na mtoa huduma anakotaka
kuhamia na kumueleza dhumuni lake.
Hatua ya pili, alisema Felician, ni kujaza fomu maalum ya maombi ya kuhamia mtandao aliotaka kuhamia.
Felician alitaja hatua ya tatu kuwa ni kujaza tamko la kukubali kuwa
mteja anakubali kuwajibika kwa madeni yoyote ambayo yanatokana na huduma
alizokuwa akipata kwa mtoa huduma wa awali kama yatakuwapo.
Felician alitaja hatua ya nne ni kuwa ni kuwasilisha kitambulisho chenye
picha ambacho kinaweza kuwa cha taifa, kadi ya mpiga kura, leseni ya
udereva, pasipoti au kitambulisho chochote rasmi kinachotambulika.
Alisema pia mteja anatakiwa kuwa na simu ya kiganjani inayofanya kazi yenye namba inayotakiwa kubaki baada ya kuhama mtandao.
Hatua ya tano, Felician alisema ni kuhamisha fedha zilizopo kwenye akaunti ya simu kabla ya kuhama ili kuepuka usumbufu.
Katika hatua ya sita, Felician alisema, mwenye namba ya simu atatakiwa
kutuma ujumbe mfupi wa maneno wenye neno HAMA kwenda namba 15080 ambayo
ni namba maalum ya kuhama.
Alisema katika hatua ya saba, mteja atapokea ujumbe mfupi wa maneno utakaomjulisha kuwa ombi lake limekubaliwa.
“Hatua ya nane, iwapo namba yako haikuzuiliwa au kusimamishwa kwa muda
kutokana na kutokamilisha malipo ya madeni ya mtoa huduma wako wa awali,
maombi yako yatashughulikiwa na utajulishwa kwa ujumbe mfupi wa maneno
maendeleo ya mchakato huo,” alisema Felician.
KAMA KAWAIDA
Alisema katika hatua ya tisa, mtoa huduma za simu za kiganjani atampatia mteja wake mpya laini mpya ya simu.
Hatua ya 10, Felician alisema, ni kusitishwa kwa huduma za kifedha kwa
muda mpaka namba ya mteja itakapohamishwa kwa mtoa huduma mpya. Kuanzia
hapo mwenye namba atatumia huduma za kifedha za mtandao mpya kama huduma
zipo.
Mhandisi wa Mawasiliano wa TCRA Felician alisema katika hatua ya 11,
huduma za kupiga na kupokea simu na ujumbe mfupi wa maneno zitaendelea
kama kawaida.
Alisema katika hatua ya 12, mteja atakuwa amehama mtandao mmoja kwenda
mwingine na kama patakuwa na ucheleweshaji, ni wa saa kadhaa, lakini
ndani ya siku mbili pekee.
“Wakati huo namba yako ya zamani itakuwa imehamishwa kwa mtoa huduma
wako mpya na laini yako ya awali haitatumika tena na utapokea ujumbe
mfupi wa maneno kuwa uhamaji umekamilika,” alisisitiza Felician.
Katika hatua ya 13, mteja atatakiwa kuweka laini yake aliyopewa kwenye
simu na endapo elimu zaidi itahitajika, mteja atatakiwa kwenda kwa mtoa
huduma kujua namna ya kutumia huduma hiyo mpya.
MASHARTI NA VIGEZO
Mbali na kuelezea hatua hizo za kujiunga, Felician alisema masharti na
vigezo vitavingatiwa ambavyo alivitaja kuwa ni mteja kutoweza kuhama na
namba iliyofungiwa au kusitishiwa huduma kwa walipaji wa kabla ya
huduma.
Alisema pia mteja hataweza kuhama na salio lililopo na atatakiwa kutumia
salio lake kwanza kabla ya kuhama kwani vinginevyo, litapotea.
Pia alisema mteja hataweza kuhama iwapo ana mkopo kutoka kwa mtoa huduma
wa awali, mikopo mingine kwa njia ya muda wa maongezi na pesa mtandao.
Felician alisema pia mteja hataweza kuhama iwapo namba yake inahusishwa na uhalifu na imefungiwa.
Kwa wateja wanaotumia utaratibu wa malipo baada ya kutumia huduma,
watatakiwa kulipa madeni ya matumizi yao kabla ya kuhama, alisema.
Wateja hao, watatakiwa pia kukamilisha masharti ya mkataba ya mtoa
huduma wake na kutizama masharti ya malipo kila mwezi kwa mujibu wa
mkataba kabla ya kuhama, alisema zaidi Felician.
Alisema pia wataendelea kupokea ankara za matumizi hadi namba itakapohamishiwa kwa mtoa huduma mpya.
“Utaendelea kupokea ankara ya mwisho hadi siku 60 baada ya kuhamisha namba yako," alisema Felician.
"Utapewa mpaka siku 30 za kulipa ankara hizo, vinginevyo utakuwa katika
hatari ya uhamaji wako kusitishwa au namba yako kufungiwa.”
Awali akizundua huduma hiyo, Mhandisi Kilaba alisema ili kufahamu
mtumiaji wa simu unayempigia amehama mtandao “utasikia milio miwili
kabla ya simu kuita."
"Hii milio ndiyo ambayo watu waliokuwa wanasema TCRA tumeanza kusikiliza mazungumzo ya watu, naomba muwaeleweshe Watanzania.”
Alisema kwa sasa kuna laini za simu milioni 40.1 nchini na kwamba lengo
la kuleta huduma hiyo ni kuboresha na kupanua huduma za mawasiliano
nchini.