Katibu CWT awavaa walimu
CHAMA cha Walimu (CWT) Mkoa wa Arusha kimesema walimu wasiotambua wajibu
wao wamekuwa wakichangia kuporomoka kwa ufaulu wa wanafunzi na
kuporomoka kwa elimu.
Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Veronica Mtalo, akizungumza kwa niaba
ya Katibu Mkuu wa CWT Taifa, Ezekiah Oluoch, alisema taifa linahitaji
walimu wenye ufanisi wa hali ya juu ili kutoa elimu yenye manufaa kwa
vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisema hayo wakati akifunga mafunzo kwa wakuu wa vyuo vya ualimu,
walimu na wakufunzi wa masomo ya hesabu wilayani Monduli juzi.
Alisema walimu wasiojitambua wamekuwa wakichangia kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi kutokana na kutotimiza wajibu wao ipasavyo.
“Walimu ni watu muhimu sana, hivyo wasipojitambua ni janga kwa taifa na
natoa wito kwa walimu watumie taaluma yao vizuri kwa maendeleo ya elimu
ya Tanzania.”
"Ni vizuri kila mwalimu akajiendeleza zaidi na kuachana na mitandao
michafu na badala yake mjikite kwenye kutafuta mitandao yenye maendeleo
ili muwe walimu bobezi," alisema.
Mtalo alisema baadhi ya walimu wameacha nafasi ya ulezi na kusababisha wanafunzi kuwa na mienendo isiyofaa.
“Mwalimu anatakiwa kufundisha kwa upendo, anatatakiwa kujiendeleza siku
hadi siku, ila sababu wengi hatujitambui tunabaki kulia mshahara mdogo,
hapana pamoja na mshahara mdogo jiongezeni zaidi ili muwe mwalimu wa
kisasa,” alisema.
Naye meneja mradi wa uboreshaji wa elimu kwa shule za msingi, Donatian
Marusu, alisema mradi wa kuelimisha walimu bobezi wa masomo ya hesabu
una lengo la kuwafikia walimu wa shule zote mkoani hapa.