-->

BILIONI 1.3 WALIZOLIPWA WANAFUNZI HEWA 2016 ZARUDISHWA BODI YA MKOPO

WAKATI wanafunzi 66,000 wa mwaka wa kwanza wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu nchini wakiwa kwenye hatihati ya kukosa mikopo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, imesema Sh. bilioni 1.3 zilizolipwa kwa wanafunzi hewa zimerudhishwa na vyuo kwenye Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi
Agosti, mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,
Profesa Joyce Ndalichako, alisema vyuo 32 vimelipa Sh. bilioni 3.58 kwa wanafunzi hewa 2,192 na kuvitaka kuzirejesha bodi.
Akizungumza mjini hapa jana kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila, alisema baada ya serikali kuagizwa fedha hizo kurejeshwa, bodi iliviandikia vyuo husika barua na baadhi vilirejesha na baadhi bado.
Profesa Msanjila ambaye anayesimamia elimu ya juu, alisema baadhi ya vyuo vilitoa maelezo na kuthibitisha kwamba fedha hizo zilitolewa kwa wanafunzi wanaostahili.
Kutokana na hali hiyo, alisema kati ya Sh. bilioni 3.58 zilizodhaniwa kutolewa kwa wanafunzi hewa, ilibainika Sh. Bilioni 1.66 zilitolewa kwa wanufaika halali.
Alisema kwa vyuo ambavyo bado havijarejesha fedha hizo au kuthibitisha uhalali wa wanafunzi waliowalipa, bodi itakata Sh. milioni 690 kwenye fedha ambazo zilikuwa zipelekwe kwenye vyuo hivyo kwa ajili ya ada.
Profesa Msanjila aliyekuwa akiwasilisha hoja ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya mwaka 2002 ya bodi hiyo, alisema HESLB bado inakabiliwa na changamoto katika kutekeleza majukumu yake, hasa marejesho ya mikopo miongoni mwa wanafaika.
Alisema waajiri wengi bado hawatoi ushirikiano wa kutosha katika kuwatambua waajiriwa wanaodaiwa na bodi.
“Baadhi ya wadaiwa wamekuwa wakibadilisha majina ili kukwepa kurudisha fedha na ili kukabiliana na hali hii, bodi imeandaa mfumo maalum ujulikanao kama ‘Online Loan Application and Management System (OLAMS),” alisema.
Profesa Msanjila alisema mfumo huo utamwezesha mdaiwa au mwajiri kupata au kuwasilisha taarifa za mdaiwa moja kwa moja kwenye bodi ya mikopo. Alisema mfumo huo utaanza kazi hivi karibuni.
Wakichangia katika kamati hiyo, wajumbe waliitaka bodi kutengeneza mfumo mzuri zaidi ili kuhakikisha fedha inayotolewa na serikali inarudishwa kwa wakati na pia ifanye marekebisho kwenye baadhi ya vifungu vya sheria husika ili kuwapa wanufaika muda mzuri wa kuanza kurejesha fedha pindi wanapoajiriwa.
Mbunge wa Bahi, Omar Badwel, alisema fedha hizo si sadaka, hivyo ni vyema zikarejeshwa ili serikali iwasaidie wanafunzi wengine.
Naye Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi, aliitahadharisha bodi hiyo kuwa makini na mabadiliko ya majina kwa wanufaika pindi wanapoolewa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Najma Murtaza Giga, aliagiza bodi hiyo kuweka mfumo mzuri wa kuwapata wanafunzi ambao hasa ni wahitaji wa mikopo kwa kuwa wengine wamekuwa wakipatiwa wakati wana uwezo.

Read also-: