Walimu Kuajiriwa Hivi Karibuni

OFISI
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imesema hadi
kufikia Juni 30 mwaka huu inatarajia kuajiri walimu 6,000 wa masomo ya
Hisabati na Sayansi kwa ajili ya shule za sekondari nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais
(Tamisemi), Joseph Kakunda, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la
Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali, ambaye alitaka kujua mikakati ya
serikali katika kuondoa changamoto katika shule za kata ikiwamo
upunguzu wa walimu wa Hisabati na Sayansi.
Pia, Bobali alitaka kujua msimamo wa serikali kuhusu wananchi kuchangia
kwenye chakula ambacho wameona ndio chachu ya kuongeza ufaulu kwa
wanafunzi katika Mkoa wa Lindi. Alisema hadi Desemba mwaka 2017,
Serikali ilikuwa imeajiri walimu 200 wa Hisabati na Sayansi kwa ajili ya
shule za sekondari.
Kadhalika, alisema serikali haijazuia wananchi kuchangia maendeleo ya
shule walichokataza ni kumzuia kumpa adha ya kukosa masomo mwanafunzi
ambaye ameshindwa kuchangia michango hiyo.
Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua kama serikali imefanya
tathmini juu ya ubora na changamoto zilizopo katika shule za sekondari
za kata nchini.
Akijibu Kakunda alisema hadi Oktoba 2017, Shule za kata 3,103 zilikuwa
na wanafunzi 197,663 ambao kama zisinge kuwepo wangeikosa elimu ya
sekondari.
Kakunda alisema maamuzi ya kuanzishwa kwa shule ya sekondari kila kata
ili kuhakikisha watoto wengi zaidi waliokuwa wanakosa nafasi za masomo
ya sekondari licha ya kufaulu mitihani ya darasa la saba kwa sababu tu
ya uchache wa shule wanapata nafasi hizo.
Alisema tathmini mbili za serikali zilizochambua kwa kina sekta ya Elimu
kupitia Tume ya Prof. Mchome ya mwaka 2013, iliyochambua sababu za
ufaulu hafifu wa wanafunzi kwenye mitihani ya mwaka 2012 na kamati ya
kuhuisha na kuoanisha sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Sera ya
Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya mwaka 1996.
Pia alisema sera ya Taifa ya Elimu ya juu ya mwaka 1999 na Sera ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa elimu ya msingi ya mwaka 2007,
iliyoongozwa na Mwalimu Abubakar Rajab mwaka 2013, ndizo zilizobaini na
kuishauri serikali kuanzisha sera mpya moja ya Elimu na Mafunzo ya mwaka
2014.
“Sera mpya imetoa maelekezo mahususi kuhusu namna ya kuboresha elimu ya
awali, msingi, sekondari, elimu ya ufundi na elimu ya juu na mitaala
imesharekebishwa, ikama, vifaa, samani na miundombinu vyote vinaendelea
kuboreshwa,” alisema.
Nipashe: